• Breaking News

    Faida ya Kumtumikia Mungu


     FAIDA ZA KUMTUMIKIA MUNGU WA KWELI

     Mkristo akimtumikia Mungu kwa bidii kuna faida nyingi katika maisha yake. Hapa nitazitaja baadhi ya faida ambazo ni kama ifuatavyo;

    1. Ataheshimika mbele ya Mungu. Ndio maana Yesu alisema;

    Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, Baba atamheshimu. Yohana 12:26


    2. Atakuwa ni rafiki wa Mungu.

    "Maandiko yale yakatimizwa yaliyonena, Ibrahimu alimwamini Mungu, ikahesabiwa kwake kuwa ni haki; naye aliitwa rafiki wa Mungu. Yakobo 2:23. Ibrahimu aliweza kuwa rafiki wa Mungu kwa sababu alikuwa anampenda na kumtumikia.


    3. Atatumiwa na Mungu kutenda mambo makuu ambayo kwa mwanadamu hayawezeka. Ndio maana imeandikwa;

    "Kwa msaada wa Mungu tutatenda makuu,.." Zaburi 60:12.


    4. Atakuwa ni mtu anayeishi katika nguvu za Roho Mtakatifu. "Na sisi tu mashahidi wa mambo haya, pamoja na Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wote wamtiio." Matendo ya Mitume 5:32. Mitume walikuwa na ushahidi ya kwamba waliopewa Roho Mtakatifu ni wale ambao wamemtii Mungu katika maisha yao. Ina naana ya kwamba wale ambao hawakumtii Mungu hawawezi kumpokea Roho Mtakatifu.


    5. Atakuwa ni mtu mwenye aman na furaha. "Wana amani nyingi waipendao sheria yako, Wala hawana la kuwakwaza."  Zaburi 119:165. 

    "Kwa maana naifurahia sheria ya Mungu kwa utu wa ndani," Warumi 7:22. Kwa hiyo mtu anaweza kuwa amani na furaha iwapo  anaipenda sheria ya Mungu na kuishi inavyosema. Kwa sababu hiyo tunaweza kuona amani  na furaha ya kweli katika Mungu haipatikani katika fedha na mali.


    6. Atakuwa ni mtu mwenye neema ya Mungu. Kwa hiyo Mungu anasema; "Na itakuwa ya kwamba, kabla hawajaomba, nitajibu; na wakiwa katika kunena, nitasikia."  Isaya 65:24.  Kwa hiyo mtu aliye na neema ya Mungu ni yule anayemtafuta Mungu siku zote na kumpendeza katika maisha yake. Kwa sababu hiyo mtu wa nanna hiyo kabla ya kumwomba Mungu hujibiwa; na ikiwa amenena tu atamsikia.


    7. Atakuwa ni mtu anayependwa na Mungu. "Nawapenda wale wanipendao, Na wale wanitafutao kwa bidii wataniona." Mithali 8:17


    8. Atakuwa ni mtu aliyebarikiwa. Mtu ambaye amebarikiwa ni yule ambaye anampenda Mungu na kulitii  neno lake.

    "kumpenda BWANA, Mungu wako, kuitii sauti yake, na kushikamana naye; kwani hiyo ndiyo uzima wako, na wingi wa siku zako; upate kukaa katika nchi BWANA aliyowaapia baba zako, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kuwa atawapa." Kumbukumbu la Torati 30:20.


    9. Atakuwa ni mtu mwenye haki. "Nuru imemzukia mwenye haki, Na furaha wanyofu wa moyo." Zaburi 97:11. Aliye na moyo mnyofu ni mtu yule ambaye ni mkamilifu. Kwa kuelezea zaidi ni mtu ambaye hana hila ndani yake. Ndio maana Yesu alipomwona Nathanaeli akimjia alimtambua rohoni ya kuwa ni mtu wa namna gani! Ndio maana imeandikwa; "Basi Yesu akamwona Nathanaeli anakuja kwake, akanena habari zake, Tazama, Mwisraeli kweli kweli, hamna hila ndani yake." Yohana1:47.


    10. Atakuwa anawezeshwa na Mungu katika mambo yote. Ndio maana Mtume paulo alisema "Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu" Wafilipi 4:13.


    11. Atakuwa ni mtu aliye karibu sana na Mungu. "Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili." Yakobo 4:8. Andiko hili linaonesha wazi ya kwamba mtu anayemkaribia Mungu ni yule ambaye ametakaswa.


    12. Bwana atamfunulia mambo yajayo. "Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake." Yohana 16:13.


    13. Bwana atamlinda na kumpigania. Ndiyo maana  imeandikwa; 

     "Malaika wa BWANA hufanya kituo, Akiwazungukia wamchao na kuwaokoa." Zaburi 34:7 


     Ni Mimi Mch Festo Mahinyila 

    Simu 0764 446 608

    E-mail fmahinyila08@gmail.com

    No comments